Huenda wizara ya barabara na kazi za umma kwenye serikali ya kaunti ya Nyamira ikalazimika kufutilia mbali leseni za kuhudumu kwa wanakandarasi wanaokarabati barabara iwapo wanakandarasi hao hawatofanya kazi zao kwa njia ya kuridhisha. 

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza siku ya Jumanne wakati alipoenda kukagua ukarabati wa barabara ya Mosobeti-Esani bila kutarajiwa, mwenyekiti wa kamati ya barabara kwenye kaunti ya Nyamira Benson Sironga aliwaonya vikali wanakandarasi kutoafikia matakwa yaliyowekwa kwenye ukarabati wa barabara.

Aidha, aliongezea kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia hali mbovu ya kukarabatiwa barabara, hali aliyosema huenda ikaigharimu serikali ya kaunti hiyo pesa nyingi ili kuzikarabati barabara hizo upya.

"Tumekuwa tukipokea lalama za wananchi kuhusiana na hali mbovu ya kukarabatiwa barabara na wanakandarasi, barabara zinazotumia pesa za umma ili kukarabatiwa na baada ya muda mfupi unapata kuwa barabara hizo zimeharibika tena," alionya Sironga. 

Sironga ameongeza kwa kusema kuwa bunge la kaunti hiyo litahakikisha kwamba wanakandarasi wanaofanya kazi duni hawalipwi pesa zao hadi pale watakapoafikia matakwa yaliyowekwa na bunge pamoja na serikali ya kaunti. 

"Kama bunge la kaunti tutahakikisha kuwa wanakandarasi wanaofanya kazi zisizoridhisha kamwe hawalipwi mishahara yao hadi pale watakapoafikia matakwa yaliyowekwa," alionya Sironga. 

Mwakilishi huyo wa wadi vilevile alisema kuwa tayari wanakandarasi wawili wamefutiliwa mbali na bunge la kaunti hiyo, ila akasema kuwa hilo litawekwa wazi kwa umma wakati kamati hiyo itakapofanya kikao tarehe tatu Novemba mwaka huu. 

"Tayari kamati ya barabara kwenye bunge la kaunti ya Nyamira imewaonyesha mlango wanakandarasi wawili na hilo litawekwa wazi kwa umma wakati kamati yetu itakapofanya kikao jumatatu tarehe tatu mwezi ujao," alisema Sironga.