Kufuatia serikali ya Kaunti ya Nyamira kununua magari na tinga tinga za kukarabati na kujenga barabara, wanakandarasi kutoka kaunti hiyo wamepongeza serikali ya kaunti hiyo kwa kuchukua hatua hiyo.
Jumuia ya wanakandarasi 'Nyamira County Contractors Association', walisema kuwa kaunti hiyo imefanya vizuri ikizingatiwa kuwa kwa muda wa miaka mitatu sasa, tangu serikali hiyo kuapishwa, wamekuwa wakikodisha mitambo na vifaa vya kujengea na kukarabatia barabara.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao George Morara, wanakandarasi hao waliahidi kushirikiana na serikali hiyo kufanikisha miradi mbali mbali ya kaunti hasa ujenzi wa barabara za kaunti hiyo ambazo ni mbovu mno.
"Tupo tayari kushikana mikono ili kuendeleza kaunti yetu na tunapongeza kaunti yetu kwa kununua vifaa hivyo vya kukarabati na kutengeneza barabara. Serikali ya kaunti itapata ushuru kupitia kukodisha mitambo hiyo kwa kulipia ada," alisema Morara.
Kiongozi huyo pia aliitaka serikali hiyo ya Nyamira kukaza kamba kwa kukabiliana na masuala ya ufisadi ambayo yamekuwa yakiendelea, kama njia moja ya kuleta uwazi baada ya wakazi wengi kulalamikia jinsi serikali hiyo inavyotumia hela za umma.