Wanakandarasi wanaokarabati barabara ya Mau Summit-Kericho wameitaka bodi ya kitaifa ya kusimamia usalama barabarani kuwachukulia hatua kali za kisheria wezi wa ishara za barabarani kwani kungo’lewa kwa ishara hizo kunachangia ongezeko la ajali.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wamesema hata kabla ya barabara hiyo kukamilika, baadhi ya ishara za barabara zimetolewa, jambo ambalo linatatiza wahandisi wa kampuni pamoja na madereva wanaotumia barabara hiyo.

Mhandisi Dori Antohi wa kampuni ya Solel Boneh International (SBI) amesema licha ya mradi wa kujenga barabara hiyo kuwa na lengo la kuwanufaisha wananchi, haswa wafanyibiashara wanao safirisha bidhaa masafa marefu, bado wananchi wanaharibu alama za barabara hiyo na kuhatarisha maisha ya wasafiri.

Amesema mtindo wa kuharibu vifaa pamoja na alama za barabara umeonekana kuendelea kwenye barabara ya Kericho –Kisumu, ambapo kampuni hiyo imekuwa ikitatizwa na hatua ya wananchi ambao hata hubalisha ishara za vipimo vya barabara na kutatiza wahandisi.

Antohi amedokeza kuwa kampuni hiyo imetoa riporti kwa maafisa wa usalama katika kaunti husika, ili hatua za kisheria zichukuliwe na pia kuuliza voingozi kuwashauri wananchi kukumbatia miradi ya maendeleo badala ya kuvuruga wawekezaji kwa lalama ambazo hazina msingi.