Wanakandarasi wanaohusika na unganishaji wa nyaya za umeme katika Kanda ya Pwani wameonya dhidi ya kutumia njia za mkato.
Menaja wa Kampuni ya kusambaza umme nchini KPLC, Hezekiah Mwalwala, amesema kuwa hatua hiyo imechangia kushuhudiwa kwa visa vya mauaji vinavyotokana na uunganishaji duni wa nyaya za umme.
Akizungumza katika kongamano la kujadili usalama wa wakaazi kupitia nguvu za umeme mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Mwalwala alisema kuwa lazima wanakandarasi hao kuhakikisha kuwa wanatumia vifaa vya kisasa kutoa huduma zinazostahili kwa wakaazi.
"Wanakandarasi wanaounganisha umeme kwa njia ya mkato bila ya kuzingatia sheria watachukuliwa hatua kwa sababu hao ndio wanachangia maafa katika maeneo ya maakazi,” alisema Mwalwala.
Kwa upande wake, Meneja wa Usalama, Afya na Mazingira ya umeme, John Guda alisema kuwa kampuni hiyo inachunguza wanakandarasi wanaonganisha nguvu za umeme kinyume cha sharia.
Aidha, aliahidi kuimarisha uhusiano bora baina ya wasimamizi wa kampuni hiyo na wanakandarasi hao.
Waliohughuria kongamano hilo pia walijadili maswala ya usambazaji wa nguvu za umeme katika taasisi mbalimbali na maeneo ya wakaazi.