Halmashauri ya ujenzi wa barabara katika eneo la Nyanza imetakiwa kuhakikisha kuwa wanakandarasi waliopewa kandarasi za kukarabati barabaraba kwenye maeneo mbali mbali jijini Kisumu wanazifanyia barabara hizo marekebisho kabla ya kuanza kwa kongamano la magavana, litakaloandaliwa jijini Kisumu baadaye mwezi huu.
Kwenye barua iliyotiwa sahihi na gavana wa jimbo la Kisumu Jack Ranguma, halmashauri hiyo imetakiwa kutoa wito kwa wanakandarasi husika kuhakikisha kuwa barabara husika zinakarabatiwa upesi, ili kuzuia msongamano wa magari wakati wa kongamano hilo.
Miongoni mwa barabara zinazotakiwa kufanyiwa ukarabati kwa haraka ni Obote, Jomo Kenyatta, katika mzunguko ulio karibu na shule ya upili ya wavulana ya Kisumu, na ile ya Paul Mboya kutokea kituo cha kuzima moto kuelekea barabara ya Obote.
“Barabara husika zinafaa kuwa tayari kutumika kufikia tarehe 15 mwezi huu,” inasema barua hiyo iliyoandikwa tarehe nane mwezi huu.
Kongamano hilo la magavana litakaloandaliwa kwenye chuo cha leba cha Tom Mboya kati ya tarehe 21 na 24 mwezi huu, linatazamiwa kufaidi uchumi wa Kisumu, huku wafanyabiashara wakihimizwa kutumia fursa hiyo kuinua biashara zao.
Kongamano hilo litajiri majuma kadhaa baada ya baadhi ya magvana kutajwa kwenye orodha ya Tume ya Maadili na Vita dhidi ya Ufisadi nchini, kufuatia tuhuma za kushiriki ufisadi.
Miongoni mwa magavana hao ni gavana wa Bomet aliye pia mwenyekiti wa baraza la magavana nchini Isaack Ruto, Evans Kidero wa Nairobi, Cyprian Awiti wa Homabay na Zachary Obado wa Migori.