Wanakandarasi katika Kaunti ya Kisii wamewalaumu wawakilishi wa wadi kwa kuwa vizingiti kwao kufanya kazi yao wanapopewa au wanapoweka maombi yao.
Kundi la wanakandarasi zaidi ya thelathini ambao walikusanyika katika mkahawa mmoja mjini Kisii, walionyesha gadhabu yao kuhusiana na walichokitaja kama kudhulumiwa na wawakilishi hao wa wadi, kwa kuwaitisha hongo ili wakubali ombi la mwanakandarasi yeyote kufanya kazi katika eneo lake.
Wakiongozwa na Ken Mariera, wanadai kuwa wawakilishi hao wamejitwika jukumu la bodi inayosimamia ukadiriaji wa utendakazi na upeanaji wa kandarasi, hasa za kuchimba barabara ambapo wao ndio hutekeleza kila wajibu isivyo kisheria.
Kulingana na Mariera, kuna baadhi ya wanasiasa hao ambao wamewasilisha kampuni zao na za wendani wao kufanya kazi sehemu zao, kisha baadaye wanaidhinisha wao wenyewe na malipo yanafanywa bila njia mwafaka kutumika.
Wamemtaka gavana wa kaunti ya kisii James Ongwae kushikilia hatamu kwa umakinifu mwingi, kwani vitisho wanavyokuwa navyo kisiasa havifai kumfanya kutosimamia ukweli,
“Kama wanamtishia kumwondoa mamlakani kwa kuwa anasimamia ukweli kuhusiana na upeanaji wa kandarasi, basi sisi wananchi tutawapata kwa debe,” alisema Mariera.
Mwakilishi wa bunge la Kisii Charles Onchong’a ameyatupilia mbali madai hayo, huku akisema kuwa ni wanakandarasi wanaohitimu ndio wanaopokea kazi, huku mwenzake kutoka eneo la Keumbu Kennedy Nyakundi akisema kuwa sharti wawakilishi wa wadi wawe macho ya wananchi kwa miradi yoyote inayofanywa na kaunti kama viongozi wao.