Wananchi na washikadau kutoka mashirika mbalimbali hii leo walikusanyika katika ukumbi wa Kaunti ya Uasin Gishu, kujadili kuhusu bajeti ya mwaka wa 2015/2016, na kutoa mapendekezo yao kuhusu namna fedha hizo zitakavyotumika.

Share news tips with us here at Hivisasa

Aidha, waziri wa fedha Bw.Shadrak Sambai alidokeza kuwa serikali kuu imeahidi kutoa pesa takriban shilingi bilioni mia mbili na themanini na tatu kwa kila kaunti, na kujua vile watakavyotumia katika kila wizara.

Vile vile aliongeza kuwa jumla ya fedha ambazo kaunti hii ilikua inahitaji ilikua shilingi bilioni tano nukta mbili, na wakapewa bilioni tano na milioni nne.

Hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa na makatibu kutoka wizara ya ardhi, kilimo, mauzo na fedha ilivutia hisia mbalimbali haswa upande wa ardhi.

Akizungumza na wananchi hao, Bi.Getrude Rabong’o, ambaye anasimamia maswala ya upangaji wa kaunti hii alisema kwamba wanajitahidi kama wizara ilikuhakikisha kuwa ardhi ya kaunti inatumika vyema kwa maswala ya kimaendeleo.

Alisema kuwa mwaka wa 2013/2014 katika kalenda ya fedha waliweza kununua ardhi katika mtaa wa Langas, itakayotumika kujengea chuo cha anwayi cha kaunti hii, ununuzi wa vifaa na ukarabati wa nyumba katika mtaa wa Elgon view.

Kando na hayo, Bi huyo aliongeza kuwa kuna miradi ambazo zinaendelea kwa sasa, zikiwemo ukarabati wa nyumba ishirini na moja katika mtaa wa Elgon view, kununua magari matatu ya wizara mbalimbali, kuhakikisha kwamba stakabadhi zote za ardhi ziko sawa na zile za serikali kuu miongoni mwa mengineo.