Shughuli za kawaida zilikwama katika eneo la Cheponde katika tarafa ya Elburgon, baada ya wananchi wenye ghadhabu kuvamia makazi ya mshukiwa wa upishi wa pombe haramu na kuyachoma.
Wananchi hao waliojawa na hasira walichoma mali ya thamani isiyojulikana, magari mawili aina , kondoo pamoja na ng’ombe ambao waliteketea wakiwa zizini.
Wenyeji hao ambao wamesema hawajuti baada ya kuchukua hatua hiyo wameelekeza kidole cha lawama kwa maafisa wa polisi katika eneo la Elburgon, kwa kumkinga mpishi huyo wa pombe haramu licha ya madhara ambayo pombe hiyo imesababishia kijiji hicho.
“Ukiona tukiwa na hasira hivyo ni sababu ya maafa ambayo yamesababishwa na chang’aa, juzi Jamaa wa miaka 36 alilewa hii pombe pamoja na bangi. Yale mambo alifanya hayaelezeki katika kijiji hiki. Alimchapa mamake mzazi na kisha kumnajisi. Mamake anatibiwa katika hospitali ya mkoa,” alisema mkazi mmoja.
Wamesema maafisa wa polisi hupokea hongo kutoka kwa jamaa huyo, wakisema wiki jana maafisa wa polisi walitifua maandamano yaliyopangwa na kina mama dhidi ya mshukiwa huyo.
Wamesema wazee kwa vijana wamepotelea katika hadaki hilo, huku wakiongeza kuwa zaidi ya watu 10 wamefariki baada ya kubugia pombe hiyo haramu tangu mwaka jana.
“Tumepoteza zaidi ya watu 10 kwa sababu ya pombe, ulevi..ulevi ulevi. Kwanzia sasa, ile hongo alikuwa anawapa polisi hapati ng’o,” aliongezea mkaazi mwingine.
Hata hivyo, Jamaa huyo amesema yeye huuza pombe halali na ambayo amepata leseni kutoka kwa mamlaka husika, huku akiongezea kuwa wakazi walifeli kwa kuchukua hatua mikononi mwao.
Wakati wa purukushani hiyo, watu watatu wakiwemo wanawake wawili na mwanaume mmoja walitiwa nguvuni na maafisa wa polisi na wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Elburgon.