Share news tips with us here at Hivisasa

Zoezi la uandikishaji wapiga kura limeng’oa nanga Jumatatu katika eneo bunge la Bahati kaunti ya Nakuru, huku wapiga kura kadri wakijitokeza katika vituo vya kujiadikisha.

Katika kituo cha kupigia kura cha Kiamaina kilicho katika ofisi za kaunti ndogo ya Bahati, jumla ya watu 17 walikuwa wameandikishwa na maafisa wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kufikia Jumatatu saa tano, watano kati yao wakiwa ni wale waliotaka kubadilisha vituo vyao vya kupigia kura vya awali, hadi Bahati. Wengine walitoka Nairobi na Kakamega.

Afisa anayesimamia zoezi hilo katika eneo bunge la Bahati bi Agnes Muriuki, alisema hiyo ni idadi ya kuridhisha chini ya saa tatu peke yake  ikizingatiwa ni siku ya kwanza.

“Tulifungua ofisi mwendo wa saa mbili, na tutafanya kazi siku saba kwa wiki. Watu walianza kuja kujiandikisha mwendo wa saa tatu, na sasa tumesajili watu 12, na wengine watano wakahamisha maeneo yao ya kupiga kura, na idadi hiyo itakuwa ya juu katika vituo vyote kufikia jioni” akasema bii Agnes akizungumza na mwandishi huyu afisini hiyo.

Kulingana na afisa huyo, IEBC inatumia maofisa wenye ufahamu wa hali ya juu ikizingatiwa usajili wa sasa wa wapiga kura unatumia mashine za kielekroniki, maarufu kama BVR.

“Tunashirikiana na ofisi ya vitambulisho hapa Kiamaina, ili mtu akichukua kitambulisho pia anaingia katika ofisi yetu na tunamsajili pia. Hapa Bahati tuna takriban maofisa 20 wa nyanjani, na tunalenga kusajili sio chini ya wapiga kura elfu 18 Bahati,” alisema Bii Agnes.

Hata hivyo changamoto ambayo mwandishi huyu alishuhudia ni uhaba wa mabango ya matangazo, ambayo kwa kawaida hutumika wakati kama huu wa kupiga kura kutangazia raia kuhusu zoezi hilo katika vituo vya kibiashara, ofisi za umma, shule na makanisa.

“Kama maafisa wa IEBC, tumefungua kurasa za mitandao ili kuwafikia wakenya zaidi kuja kujiandikisha kama wapiga kura, kupitia Facebook na Twitter. 

Tusaidieni kusambaza habari hizo pia kupitia IEBC Bahati kwenye Facebook, na IEBC Bahati_Naku; kwenye twitter.”