Mwakilishi wa wadi ya Bokeira Karen Atuya amewaomba wakazi wa wadi yake kuwa na subira kuhusiana na kukarabatiwa barabara za eneo hilo kwa kuwa mradi huo ulisitishwa kwa muda kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika maeneo mengi nchini.
Kulingana na Atuya, barabara ambazo zilikuwa zimelimwa zikingoja kuezekwa mchanga haziwezi kuendelea kukarabatiwa kwa sababu ya mvua hiyo inayoendelea kunyesha.
"Mvua kubwa inayoendelea kunyesha imesababisha tusitishe shughuli za kukarabati barabara ya Nyakaranga-Matongo na ile ya Enchoro, na hii ni kwa sababu ninahofia kuwa huenda maji ya mvua yakasomba mchanga unaotumika kukarabati barabara hizo hata kabla hatujamaliza kuzikarabati," alisema Atuya.
Akizungumzia swala la kuimarisha usalama wa wananchi, mwakilishi huyo alisema kuwa yafaa maafisa wa polisi wa utawala washirikiane na wananchi ili kuhakikisha kuwa doria zinaimarishwa hasa usiku ili kuwalinda wenyeji kutokana na visa vya uhalifu.
"Nawaomba maafisa wa polisi wa utawala kwa ushirikiano na wananchi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wanaimarisha doria hasa nyakati za usiku kama njia mojawapo ya kuwahakikishia wenyeji usalama wao," alisema Atuya.
Atuya aidha aliwaomba vijana wajiunge na makundi ya kujistawisha ili waweze kuomba mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha ili waanzishe biashara zao badala ya kujihuzisha na wizi.
"Nawaomba vijana wajiunge kwenye makundi ya kujistawisha ili waweze kuomba mikopo kutoka kwa mashirika ya kifedha hasa benki ili waanzishe biashara badala ya kujihuzisha na wizi," aliomba Atuya.