Muungano wa wanaoendesha Bodaboda kutoka Kaunti ya Kisii wamepinga vikali sheria mpya zilizotolewa wiki jana na Mamlaka ya Uchukuzi Kenya almaarufu NTSA.

Share news tips with us here at Hivisasa

Sheria hizo ambazo zinawataka wahudumu wote wa Bodaboda kuwa na kofia mbili (yake na abiria), koti za mwako na wasizidishe abiria mmoja, hazijapokelewa vizuri na wahusika wakuu wakidai kuwa Serikali haikuwahusisha katika maamuzi hayo.

Kupitia kwa Mwenyekiti wa wenye Bodaboda hao kutoka Kisii Mike Mose amesema kuwa sheria hizo zitawafinya zaidi ukizingatiwa kuwa wengi wa vijana hujimudu kupitia biashara hiyo ya Bodaboda.

“Kama sasa hivi wanabeba angalau abiria wawili na maisha ni magumu hivi, seuze abiria mmoja, si watakuwa wezi," alisema Mose.

Alimuomba Mkurugenzi Mkuu wa NTSA kuwaita wawakilishi wote wa wanaoendesha Bodaboda kote nchini ili walijadili suala hilo na kupata suluhisho mwafaka wa kudumu.

Naye Benard Mukua ambaye ni Katibu Mkuu wa chama hicho cha wanaoendesha Bodaboda Kisii alihoji kuwa ni bora zaidi NTSA kuwashirikisha wahusika wote na kutaja hatua hiyo kuwa ya kiimla.

"NTSA haijafanya vizuri, wenye Bodaboda hutegemea kazi hii ya ya Bodaboda kwa asilimia 100 kwa hivyo angeturuhusu tuwe tunabeba abiria wawili, angalau tupate pesa ya kula na kulipia kodi,” alisema Mukua.

Hata hivyo viongozi hao wawili waliahidi kushughulikia suala hilo. Kwa upande wa uovu wa washirika wao, watahakikisha kuwa kuna uhusiano mwema baina ya abiria na wanaoendesha Bodaboda hao.