Wanaoendesha bodaboda kutoka wadi ya Sameta iliyoko eneo bunge la Bobasi kaunti ya Kisii wana kila sababu ya kutabasamu baada ya kupokezwa pesa za basari ili kuendelea kupata mafunzo ya uendeshaji wa pikipiki.
Wakizungumza na mwanahabari huyu siku ya Alhamisi katika uwanja wa shule ya upili ya wavulana ya Sameta, walipokuwa wakipokezwa pesa hizo, waendeshaji bodaboda hao walisema sasa wataendelea na masomo ya kujifunza uendeshaji wa pikipiki bila changamoto yoyote.
Wanaoendesha bodaboda hao walipokezwa pesa pesa hizo kutoka kwa mwakilishi wao wa wadi hiyo ya Sameta Evans Zico Obwogi ambaye alisema wengi wa wanabodaboda huendesha pikipiki bila kufunzwa na kuwa hatari wanapowabeba wateja.
“Nafurahia sana mwakilishi wetu kwa kutukumbuka sisi vijana. Nimekuwa nikiendesha pikipiki kwa mwaka mmoja bila cheti cha uendeshaji. Sasa nitarudi kwa mafunzo ingawa najua kuendesha ili nikabidhiwe cheti hicho,” alisema Erick Masira.
“Huwa tunapitia changamoto nyingi tukiwa barabarani. Maafisa wa trafiki hutushika kwa kutokuwa na cheti lakini sasa nitaenda niingie kwa mafunzo nipatiwe cheti. Mungu ambariki mwakilishi wetu na aendelee kusaidia vijana,” alisema Evans Ondigi, mwendeshaji bodaboda mwingine.
Wakati huo huo, mwakilishi huyo alisema yuko na mikakati ya kuwapeleka baadhi ya vijana kutoka eneo hilo kwa mafunzo ya kujenga nyumba na wengine awapeleke kwa mafunzo ya kuwa seremala ili vijana wa eneo hilo kujimarisha kiuchumi.