Kamati ya usalama katika eneo la Kisiwani imesema itaanzisha oparesheni ya kuwasaka wahalifu wanaopora vipuri vya magari yanayoegeshwa katika maeneo mbalimbali mjini Mombasa.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Naibu Kamishna wa Mombasa Mahmoud Salim alisema kumekuwepo na ongezeko la visa vya wizi wa vipuri vinavyoripotiwa kila mara na wamiliki magari ya kibinafsi na pia madereva wa matatu.

Akizungumza siku ya Jumamosi mjini Mombasa, Salim alisema kuwa maafisa wasio na sare za kazini wataanza kushika doria sehemu mbalimbali mjini Mombasa hususan maeneo yanayoathirika zaidi na uhalifu huo.

“Maeneo ya Kisimani na Buxton yamekuwa yakishuhudia ongezeko la visa hivyo, huku uhalifu huo ukitekelezwa wakati wa msongamano wa magari,” alisema Salim.

Aidha, Salim alikashifu tukio la siku ya Ijumaa ambapo dereva wa tuktuk alidaiwa kuwasafirisha vijana waliodaiwa kutekeleza uhalifu katika maeneo ya Buxton na King’oran.

Naibu kamishna huyo alisema kuwa idara ya usalama haitawavumilia wahudumu wa tuktuk wanaoshirikiana na wahalifu.

Uporaji wa vipuri vya magari katika maeneo mbalimbali ya mji wa Mombasa umeonekana kukithiri huku madereva wa matatu wakilalamikia kuibiwa vioo vya gari.