Shirika la Msalaba Mwekundu tawi la Mombasa limewataka wakaazi wanaoishi katika maeneo yaliyo chini kuhamia maeneo ya juu ili kuepuka athari za mafuriko wakati huu wa msimu wa mvua.
Afisa Mkuu wa shirika hilo katika Kaunti ya Mombasa Mohammed Rajab amesema kuwa mvua inayoendelea kunyesha imechangia kushuhudiwa kwa mafuriko katika maeneo mengi ya kaunti hiyo yakiwemo maeneo ya Likoni, Changamwe, Jomvu, katikati ya mji wa Mombasa na pia katika maeneo ya Bombolulu na Kisimani.
Akizungumza katika afisi za shirika hilo mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Rajab alisema kuwa kikosi cha kukabiliana na majanga na kile cha kutoa huduma ya kwanza kiko nyanjani kutoa usaidizi ili kuzuia mikasa.
“Tunawaomba wakaazi wanaoishi katika maeneo ya chini kuhama maeneo hayo ili kuepuka mafuriko hasa msimu huu wa mvua,” alisema Rajab.
Rajab aidha alisema kuwa shirika hilo linaendeleza juhudi za kusambaza dawa za kutibu maji ili kuzuia kuchipuka kwa mkurupuko wa maradhi.