Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kaunti ya Kisii ikishirikiana na chama cha Lions Club tawi la Kisii liliwafadhili watu wanaoishi na ulemavu kitimagurudumu 30 na fimbo za kutembelea.

Ufadhili huo ulifanywa na waziri wa afya katika Kaunti ya Kisii Sarah Omache na Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ambao waliahidi kuendelea kufadhili wanaoishi na ulemavu wa kaunti hiyo kama njia mojawapo ya kuwakumbuka. 

Akiongea siku ya Jumanne katika uwanja wa shule ya msingi ya Tabaka iliyoko eneo bunge la Mugirango Kusini, Omache alisema watu wanaoishi na ulemavu wanapaswa kufurahia serikali za ugatuzi.

“Tutaendelea na mradi huu wa kuwafadhili wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Kisii ili nao wafurahie matunda ya serikali ya ugatuzi kupitia kufadhiliwa kwa kitimagurudumu,” alisema Omache.

Wakati huo huo, mkewe Gavana Ongwae, Elizabeth Ongwae aliwafadhili wasichana wa shule sodo za hedhi katika shule mbalimbali za wadi ya Tabaka jambo ambalo liliweza kuwafurahisha wakaazi wa eneo hilo.

Wakaazi wa eneo hilo walimwomba Gavana James Ongwae kutengeneza barabara za wadi hiyo ambazo hazipitiki mvua inaponyesha.

“Sisi tunahitaji atengeneze barabara zote za wadi hii maana zingine zinatusumbua mvua inaponyesha. Barabara ya kutoka Nyachenge kuelekea Tabaka huwa haipitiki kunaponyesha,”alisema Moorine Osoro, mkaazi.