Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Likoni Willy Simba amewataka wanaozuru fuo za bahari mjini Mombasa kuwa waangalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya yanajiri baada ya mwili mwengine wa mwanaume mwenye umri wa makamo kupatikana ukininginia kwenye ufuo wa bahari katika eneo la Likoni.

Kulingana na Simba, huenda vijana wanaohudumu kwenye fuo za bahari wakawa wameanza tabia ya kuwalaghai wananchi wanaokwenda kujivinjari ufuoni na kuwapeleka kwenye sehemu hatari za bahari kisha kuwaacha baharini kutokana na kutoelewana.

Alisema kuwa anafahamu fika kwamba kuna baadhi ya vijana ambao hutaka kufanya mapenzi na wananchi wanaozuru bahari hindi na iwapo hawatakubali, wao huishia kuachwa kwenye bahari.

Aidha, Simba alisema kuwa mwili wa mwanafunzi uliopatikana wiki jana katika ufuo wa Hoteli ya Shelly huenda ulitumiwa kimapenzi kabla ya kutupwa baharini.

“Japo hakuna majeraha kwenye mwili wa mwanamume huyo, ni sharti sheria zifuatwe ili kubaini chanzo cha vifo vya wananchi kwenye fuo za bahari. Hali hii huenda ikaathiri sekta ya utalii ambayo kwa sasa imeanza kustawi,” alisema Simba.

Aidha, afisa huyo amewataka wananchi kuwa katika mstari mbele kutoa taarifa kuhusiana na uhalifu wa aina yoyote kwenye fuo za bahari ili kuiwezesha idara ya usalama kukabiliana na wahalifu.