Wizara ya kilimo kaunti ya Mombasa imetoa wito kwa wanaomiliki mabohari ya mazao ya shambani kuanza kununua bidhaa hizo kutoka kwa wakulima wadogowadogo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza baada ya mkutano na washikadau wa idara ya kilimo, mwenyekiti wa kamati kilimo kaunti ya Mombasa, Anthony Njaramba ambaye pia ni kaimu waziri wa kilimo kauti hii, amesema kuwa njia ya kuwatia motisha wakulima wadogo ni kuwataftia soko watakaouza bidhaa zao ili nao waweze kupata mapato mazuri ambayo kwa njia nyengine yatachangia katika mapato ya kaunti hii.

Anasema licha ya masoko ya Marikiti na Kongowea pana haja ya wanaomiliki mabohari kuanza kununua bidhaa kwa wakulima hao ili waweze kupata manufaa ya mazao yao.

Kwa upande wa wakulima, Njaramba amewataka kubuni miungano ambayo watatumia kutaftia nafasi kwenye mabohari hayo ili kuhakikisha kuwa mazao yao yanapata soko la kuaminika katika baadhi ya mabohari yanayojulikana hapa mjini Mombasa.

Akitoa mfano wa baadhi ya kampuni zinazonunua zao la mahindi, Njaramba ametaja kampuni kama vile ya Mombasa maize millers, Tss miongoni mwa nyengine kuwa hununua zao la mahindi kwa wingi na kusiaga mahindi ili kuuza unga kwa wananchi wa hapa mjini Mombasa na Kenya kwa ujumla.

Anasema iwapo wenyeji wa mabohari hayo watakubaliana na wakulima basi itakuwa bora zaidi kwani kampuni hizo hazitalazimika kutafuta mahindi nje ya kaunti hii.