Wanaoendesha Bodaboda katika eneo la Turi wameteketeza mali ya mshukiwa mmoja ambaye alivamia mmoja wao kwa upanga na kumjeruhi vibaya.
Kwa mujibu wa wenye Bodaboda hao, mshukiwa huyo anayedhaniwa huenda akawa amechanganyikiwa kimawazo alifika katika eneo ambapo wahudumu wa Bodaboda husubiri wateja na bila kusita akamvamia mmoja wao kwa upanga huku waliokuwepo wakifanikiwa kutoroka.
“Alifika katika stage yetu akisimama wima na bila kusita tukaona amevamia mmoja wetu kwa panga aliyokuwa nayo. Kuona hatari iliyokuwa ikitukodolea macho tukaamua kuhepa kabla ya maafa zaidi,’’ alisema Peter Njoroge.
Aidha, imearifiwa kuwa baada ya wahudumu wa Bodaboda kumakinika walimfuata Jamaa huyo kwa upesi lakini akafanikiwa kutoroka.
Msafara mkubwa wa wahudumu wa Bodaboda waliojawa na ghadhabu ulifululiza hadi nyumbani kwa Jamaa huyo huku wakitishia kuchoma ploti anakoishi.
Wenyeji wamesema iliwachukua muda wa nusu saa hivi kuwalai wenye Bodaboda hao kubadili nia ya kuchoma ploti hiyo na baadaye wakaamua kuvunja nyumba ya Jamaa huyo na kutoa nje mali yake yote.
Waendesha Bodaboda wengi walifika hapo kwenye ploti wakipiga kelele huku wakisema wanataka Jamaa huyo ajitokeze.
“Iwepo hatutampeana kwao huenda wakalazimika kuchoma ploti kwa kosa alilofanyia mmoja wa mahudumu hao. Hatukuweza kujua mara moja kilichokuwa kimetokea,” alisema Irene Njeri, mpangaji katika ploti hiyo.
Wakazi hao wamesema wenye Bodaboda hao walitoa kila kitu katika nyumba ya mshukiwa huyo na kuvipeleka kando ya barabara ambapo waliviteketeza vyote.
Miongoni mwa vitu vilivyoteketezwa ni pamoja na Bodaboda, baiskeli ambazo Jamaa huyo hutumia katika kufanya kazi yake ya kuchuuza viazi kutoka Turi hadi Njoro.
Maafisa wa Polisi kutoka kwenye kizuizi kilichoko kwenye barabara ya Turi kuelekea Molo walifika katika eneo la Tukio hilo lakini hawakufanikiwa kuzima moto huo wala kuokoa mali ya mshukiwa huyo.
Mwendesha Bodaboda aliyeruhiwa amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Molo ambapo anaendelea kupokea matibabu huku mshukiwa anayesakwa akiwa ameingia mafichoni.