Kampuni ya maji katika Kaunti ya Mombasa imetoa onyo kali kwa watu wanouzia wakaazi wa kaunti hiyo maji kwa bei ya juu.
Afisa katika idara ya maji na rasilimali katika serikali ya Kaunti ya Mombasa amesema kuwa uchunguzi dhidi ya watu hao unafanywa na utakapokamilika, wafanyibiashara hao watachukuliwa hatua za kisheria.
Akiongea na wanahabari siku ya Jumatano alipozuru eneo la Miritini, lililoko katika eneo bunge la Jomvu, alipokuwa akiendesha zoezi la kusitisha huduma za usambazaji maji kwa njia isio halali, Ibrahim Basafar, alisema kuwa watahakikisha kuwa wakaazi wa Mombasa wamepata maji safi kwa bei nafuu.
Aidha, afisa huyo alisema kuwa zoezi hilo la kuboresha huduma ya maji itafanywa katika maeneo mengine ikiwemo Kisauni, ambako kunadaiwa kuwa na zaidi ya vibanda 1000 za kuuza maji zisizohalali.
Suala la ukosefu wa maji limekuwa likikithiri sana katika Kaunti ya Mombasa, huku wakaazi wakilaumu serikali ya kaunti kwa kutotoa huduma duni.