Share news tips with us here at Hivisasa

Mkuu wa polisi wilayani Kisii ya kati Francis Nguli amewaonya wanaouza pombe haramu na dawa za kulevya katika kituo cha magari mjini Kisii.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa kuna baadhi ya wafanyibiashara ambao wanauza mboga katika kituo cha magari cha Kisii ambao pia wanauza pombe hiyo kisiri.

Kulingana na mkuu huyo wa polisi, madereva wa magari pamoja na utingo wao mjini Kisii huwa wanalewa baada ya kuuziwa pombe hiyo na dawa za kulevya na wafanyibiashara wa mboga walioko katika kituo hicho cha magari.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu mjini Kisii, Nguli alisema kuwa yeyote ambaye atafumaniwa akiuza pombe hiyo atachukuliwa hatua kali ya kisheria.

Jambo hilo lilimpelekea mkuu huyo wa polisi kuweka kituo cha polisi katika kituo hicho ili kukabiliana na wale wanaouza pombe hiyo.

“Kama mtu anafanya biashara, wacha afanye biashara ambayo ni halali. Haya mengine ya kujifanya kuuza mboga huku ukiuza pombe na mihadarati si halali. Yeyote atakayefumaniwa akifanya hivyo atakabiliwa kisheria,” alisema Nguli.

Maafisa hao ambao watakuwa katika kituo hicho ambacho kilichoanzishwa Jumatatu watakuwa katika kituo hicho masaa 24 ili kuhakikisha pombe hiyo na dawa za kulevya zimesitishwa.

Nguli pia alifanya msako wa pombe katika eneo la Keumbu na kuwatia mbaroni watu wannee ambao walikuwa wakitengeneza pombe haramu.