Share news tips with us here at Hivisasa

Wanasiasa kutoka eneo la Jomvu na Changamwe wamekosoa hatua ya vyama vya walimu nchini kutokubali kurudi kazini hata baada ya maamuzi ya mahakama.

Wakiongea siku ya Jumapili katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu Alidina Mombasa, mwakilishi wa wadi ya Jomvu, Karisa Nzai, alisema ni wajibu wa serikali kuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na vyama vya walimu ili kupata suluhu la swala la mgomo wa walimu nchini ambao umetatiza masomo kwa muda wa majuma manne sasa.

“Suluhu la kipekee ni mazungumzo kati ya serikali na vyama vya walimu nchini Knut na Kuppet na kurejea katika shuguhli za kawaida kimasomo ili kuafikia ruwaza ya 2030.

Mwanasiasa Omari Mburi alisema kuwa viongozi wa chama cha walimu cha Knut wamewapa walimu mwelekeo mbaya baada ya uamuzi wa mahakama kuamuru walimu nchini kusitisha mugomo huo kwa miezi mitatu.

“Walimu pia yawapasa kuitikia wito wa mahakama na kuheshimu sheria ili mahakama iwasaidie kisheria kushughulikia matakwa yenu ya kutaka nyongeza ya mishahara,” alisema Mburi.

Wakazi wa eneo hilo pia wamelalamikia kile walichikiita kuzembea kwa serikali na sekta husika kutatua mgomo wa walimu nchini na kuwafanya watoto wao kujiunga na makundi yasiyofaa.

Jared Momanyi, mzazi, alisema ni jukumu la serikali kuwajibika na kushughulikia nyongeza ya mishahara ya walimu nchini kupitia kwa jopo ya mishahara linaloogozwa na Sarah Serem.

“Watoto wetu wamo katika hatari ya kujiunga na makundi mabaya na ulevi. Sisi kama wazazi tunahofu sana na tunaiomba serikali pamoja na walimu nchini kulegeza kamba na kuafikiana ili jambo hili lisije likawa janga katika taifa letu,” alisema Momanyi.