Idara ya usalama eneo la Pwani imewaonya viongozi wa kisiasa wanaofadhili makundi ya vijana kuzua taharuki ili kuvuruga usalama wa eneo hili kuwa watakabiliwa kikamilifu.
Kamanda mkuu wa polisi eneo la Pwani Francis Wanjohi, amesema kuwa tayari maafisa wa polisi wanawachunguza baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaopanga njama hizo za kufadhali makundi ya vijana, akisema kuwa lazima hatua kali za kisheria kuchukuliwa.
Akizungumza na mwanahabari huyu afisini mwake mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Wanjohi amesema kuwa makundi ya kihalifu yanayowahangaisha wakaazi yanafadhiliwa na viongozi wa kisiasa ili kuwatia hofu wakaazi wasijihusishe moja kwa moja katika uchaguzi mkuu ujao kwa manufaa yao binafsi.
Kamanda huyo mkuu wa polisi eneo hili ameshikilia kuwa lazima usalama wa wakaazi uimarishwa na kamwe serikali hatakubali kuwepo na makundi ya kihalifu ya kuwahangaisha wakaazi huku akiahidi kuyakabili kikamilifu.
"Tumepata ripoti kamili kutoka kwa wakaazi kuwa kuna baadhi ya viongozi wa kisiasa wanafadhili makundi ya vaijana ya kihalifu kuleta wasiwasi na kufanya wananchi kususia kupiga kura wakati wa uchaguzi mkuu sisi tunasema lazima hiyo manene ikomeshe na kutawakabili kikamilifu," alisema Wanjohi.
Baadhi ya makundi yaliyotajwa kuwahangaisha wakaazi eneo hili ni pamoja na lile la The Spanish, Gaza, Wakili Wao, Wakali Kwanza na Kapenguri 6 miongoni mwa makundi mengine ya kihalifu.