Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mbunge wa eneo bunge la Kitutu Chache Kusini, Richard Onyonka, amewaonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika mradi wa NYS.

Wito huo umetolewa baada ya baadhi ya wanasiasa kusema pesa zile zinatumika kwa mradi huo wa NYS ziondolewe na kutumika kuwalipa walimu.

Onyonka alisema kuwa mradi wa NYS umewasaidia idadi kubwa ya vijana ambao wangejiingiza na masuala ya uhalifu, kwa kuwapa ajira na kuwawezesha kupata riziki ya kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumapili mjini Kisii, mbunge huyo alisema yeye kama mbunge ataendelea kuunga mkono mradi wa NYS hadi mwisho kwani mradi huo umewanasua vijana wengi kutokana na uhalifu.

“Serikali iliangalia ni mbinu ipi itatumia ili kuepusha vijana wetu na uhalifu katika vijiji mbalimbali nchini na ikaleta mradi wa NYS. Haya mengine ya wanasiasa ambao wanataka kujaribu kuingiza siasa kwa mradi huo yanatokea wapi?”auliza Onyonka.

Aliongezea, “Naomba tusiingize siasa kwa mradi huu wa NYS kwani ni wa maendeleo na umewasaidia vijana wetu kujiendeleza na kujiimarisha kimaisha na kuwaepusha na uhalifu.”

Onyoka alisema kuwa mradi huo utaendelea kuleta manufaa kwa vijana walio katika mradi huo.