Mbunge wa Changamwe Omar Mwinyi amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia vijana kuzua vurugu na kuharibu usalama wa eneo hilo.
Akizungumza katika eneo la Changamwe siku ya Jumatatu, Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo imehujumu utekelezaji wa maendeleo mashinani.
Mbunge huyo alisema kuwa lazima hali hiyo kukomeshwa.
Mwinyi amewataka wakaazi kujitenga na viongozi kama hao na kujitolea kikamilifu katika uimarishaji wa maendeleo katika eneo bunge hilo, hasa uimarishaji wa miundo msingi na usalama.
Wakati huo huo, ameikosoa serikali ya Kaunti ya Mombasa chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho, kwa madai ya kutenga eneo bunge la Changamwe, alilosema linakabiliwa na changamoto nyingi.
"Tunakosa kuelewa jinsi serikali ya Kaunti ya Mombasa imeshindwa kuwatekelezea wakaazi wa Changamwe maswala muhimu ikiwemo usambazaji wa maji safi, kuzoa taka pamoja na mambo mengine muhimu,” alisema Mwinyi.