Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mwanasiasa ambaye anaazimia kuwania kiti cha ubunge cha Emuhaya kwenye uchaguzi mkuu ujao, Reuben Akabwa amewataka viongozi walio mamlakani kwa sasa kutumia vyema fedha za Hazina ya Maendeleo ya eneo Bunge almaarufu CDF.

Akiongea kwenye hafla moja ya kuchangisha pesa kujenga choo kwenye soko la Ndiri eneo la Maseno siku ya Jumanne, Akabwa amewataka viongozi wa maeneo Bunge kwenye Kaunti ya Kisumu kutumia vyema pesa hizo kwa kuwaletea karibu wananchi maendeleo yanayotokana na pesa hizo.

Alisema kuwa wengi wao wanavuja pesa hizo za maendeleo badala ya kusitawisha miradi ya maendeleo yaliyonuiwa pesa hizo ili kufaidi raia wa eneo hilo. Aliongeza kuwa hali hiyo inarudisha nyuma maendeo katika maeneo mengi.

“Pesa nyingi zinavujwa na viongozi hawa wa maeneo Bunge badala ya kufanya maendeleo. Hali hiyo imerudisha nyuma sana maendeleo ya maeneo bunge na kutokuwafaidi wananchi,” alidai Akabwa.

Mwanasiasa huyo alishtumu sana propaganda zinazoenezwa na baadhi ya viongozi walioko mamlakani kwa kuwekelea bajeti bandia ya miradi ambazo hazijaafikiwa kwa nia ya kuvuja pesa za wananchi.

“Nawaonya viongozi waliochaguliwa na wananchi kuwafanyia kazi kwa kuchapisha ripoti bandia kwenye bajeti za miradi ambazo haziko. Hii inaonyesha wazi kuwa wameshindwa na kazi na haja yao ni kula pesa za wananchi,” aliongeza Akabwa.

Akabwa alikosoa bajeti ya mwaka 2014/15 ambapo ripoti ilitolewa kwamba Sh11M zilitumika kujenga vyoo kwenye masoko na kukarabati barabara katika Wadi nane za eneo hilo.