Wanasiasa watano kutoka kaunti za Kisii na Nyamira wamepinga vikali pendekezo la bahasha ya Waki kufunguliwa.
Bahasha hiyo ambayo ina majina ya washukiwa wa vita vya baada ya uchaguzi ni ripoti ya tume iliyowekwa kuchunguza sababu za vita hivyo.
Seneta wa kaunti ya Nyamira Kennedy Okong’o, na wabunge Jimmy Angwenyi (Kitutu Chache Kusini), Mbunge wa Bomachoge Borabu Joel Onyancha, Stephen Manoti wa Bobasi na Richard Tong’i wa Nyaribari Chache wamejitokeza na kupinga pendekezo hilo la CORD.
Seneta Okong’o alisisitiza kuwa ni muhimu kuwaleta wakenya pamoja badala ya kuwatenganisha kwa kuwarudisha kwa mambo ya 2007 na 2008 yaliyopita.
Viongozi hao walisema kuwa kufungua bahasha hiyo itakuwa ni kusumbua donda ambalo lilikuwa linapona, wakisema ni heri wanasiasa kujishughulisha na maswala ya utangamano.
Mbunge Onyancha wa Borabu Bomachoge alisema kuwa licha ya kwamba wenzake wa kutoka jamii ya Kisii waliathirika na vita hivyo, na zaidi ya watu elfu kumi kupoteza makao yao, ni bora kuwaleta wakenya pamoja.
Mheshimiwa Tong’i kwa upande wake alisema kuwa jukumu la viongozi ni kuhubiri amani na umoja na ya kuwa yeyote anayesema hoja tofauti ni mjumbe wa shetani.