Viongozi wa kisiasa mjini Nakuru wamewataka wafanyibiashara kufunga biashara zao Jumamosi ya tarehe 16 siku ambayo muungano wa Jubilee unatarajiwa kuandaa maombi ya shukrani kufuatia kufutiliwa mbali kwa kesi iliyokuwa ikimkabili naibu rais William Ruto katika mahakama ya ICC.
Viongozi hao ambao wmejumuisha wawakilishi wa kina mama na wa kisiasa walisema kuwa itakuwa heri kila shughuli ikisimama mjini Nakuru siku hiyo ili kutoa nafasi kwa maombi hayo kufanyika.
Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha TNA Abdul Noor alisema hatua hiyo itamudhihirishia naibu rais kuwa watu wa Nakuru wanampenda na wako pamoja naye.
“Sisi tungeomba tu wakaazi wa Nakuru mjini wanaofanya Biashara kufunga Biashara zao siku hiyo ili kutoa nafasi ya kuweza kufanyika kwa maombi hayo muhimu na kushirikiana na naibu rais kumshukuru Mungu kwa kuweza kusikiza maombi yao,” alisema Noor.