Viongozi wa kisiasa katika ukanda wa Pwani wametakiwa kuwahamasisha wakaazi kuhusiana na fedha mbalimbali za serikali kuu.
Hatua hiyo inanuia kuwawezesha wakaazi wa eneo hilo kuzitumia fedha hizo kuukabili umaskini.
Naibu mkurugenzi wa kituo cha kupambana na ugaidi cha 'National Counter terrorism Center’ NCTC Joseph Opondo, amesema wakaazi Pwani wanahisi kubaguliwa na kutengwa na serikali kuu.
Alisema kuwa ni kupitia fedha hizo ndipo makundi ya vijana na akina mama yataweza kuzikabili changamoto za kimaisha na kujiimarisha kiuchumi.
Akizungumza Mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Opondo alisema kwamba iwapo vijana watashirikishwa kikamilifu katika fedha hizo, basi hawatasalia mitaani wala kushawishiwa kujiunga na makundi ya kigaidi na yale ya kihalifu.
Mtaalam huyo wa maswala ya usalama nchini alisisitiza umuhimu wa viongozi wa kisiasa kuhakikisha fedha hizo zinaafikia malengo yake.
Opondo vile vile amedokeza kwamba kituo hicho cha NCTC, kinaendeleza mradi wa kuwasaidia vijana walioasi ugaidi na misimamo mikali kubadilisha tabia na kuwa watu wema.
Aidha, amewashinikiza wazazi walio na watoto wanaolenga kuyaasi maswala ya itikadi kali kujitokeza ili watoto wao wasaidiwe.
Maafisa wa kituo hicho hata hivyo wameitaka jamii ya Pwani kushirikiana na vikosi vya usalama na hasa kile cha kupambana na ugaidi nchini ili kulikomesha tatizo la itikadi kali na ugaidi miongoni mwa jamii, hususan vijana kutoka Pwani.