Wanaume 17 wameshtakiwa katika Mahakama ya Mombasa kwa madai ya kuharibu mali.
Washukiwa hao wanadaiwa kuvunja nyumba ya thamani ya shilingi laki nane na kuiba mali ya zaidi ya shilingi laki moja Jumamosi iliyopita katika eneo la Hamisi Estate, Changamwe.
Wakili wa washukiwa hao, Pascal Nabwana, aliambia mahakama siku ya Jumanne kuwa wateja wake ni waajiriwa katika kampuni moja ya madalali na kwamba walikamatwa wakitekeleza wajibu wao.
Nabwana aliiomba mahakama iwaachilie kwa dhamana ya chini kwa kuwa walipaswa kulipwa shilingi 300 kwa kazi hiyo mbali na kutegemewa na familia zao.
Hakimu Daniel Ogoti aliagiza washukiwa hao waachiliwe kwa dhamana ya shilingi elfu tano kila mmoja.
Kesi hiyo itatajwa tarehe 18 mwezi Mei.