Mbunge wa Kisumu ya Kati Ken Obura, amewaonya vijana wa kiume wanaohudumu kwenye mradi wa vijana wa Huduma Kwa Taifa - NYS, dhidi ya kile anachosema tabia ya kuwatongoza wake wa wenyewe.
Obura alisema kwamba amepokea malalamishi chungu nzima kutoka kwa baadhi ya wanaume, wanaodai kwamba vijana wa kiume waliochaguliwa kusaidiana na maafisa wa NYS kusafisha mitaa ya mabanda ya Obunga, Nyalenda na Manyatta jijini Kisumu, wanawanyemelea wanawake wanaofanya kazi nao, na ambao tayari wameolewa.
“Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa wanaume kwamba wake wao hawarudi nyumbani baada ya kazi, na kuwa wanahepa na wasimamizi wa NYS ili kunufaika kifedha,” alisema mbunge huyo.
Mbunge huyo alisema kuwa malalamishi hayo, yanachafua jina zuri la mradi huo wa NYS.
“Ni ukiukaji wa maadili kwa vijana wa NYS kutongoza wake wa watu. Jukumu lao ni kuongoza, kusaidia na kusimamia wanawake hao ambao wamejitolea kufanya kazi ili kujikimu maishani,” alisema Obura.
Mbunge huyo alisema hayo mtaani Nyalenda jijini Kisumu mwishoni mwa juma, wakati wa uzinduzi wa mradi wa kusafisha mitaa ya Obunga, Nyalenda na Manyatta unao-ongozwa na vijana wa NYS.
Vijana zaidi ya 4, 000 katika mitaa hiyo, wameajiriwa kwenye mradi huo katika mitaa hiyo mitatu.
Kazi ya kusafisha mitaa hiyo, ilianza rasmi Jumatatu tarehe tisa mwezi huu.