Licha ya unyanyapaa unaotokana na dhulma za kijinsia, wanaume katika ukanda wa Pwani na nchini kwa jumla wametakiwa kujitokeza na kuripoti visa hivyo.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kulingana na Shitemi Khamadi, afisa kutoka shirika la kutoa hamasa kwa jamii la Pawa254, visa vya wanaume kudhulumiwa kimapenzi vimeonekana kuongezeka ila wengi wamesusia kutoa taarifa.

Shitemi amedokeza kuwa visa vingi vya dhulma za kijinsia haswa vya ulawiti vimekithiri miongoni mwa wanaume, ila wengi wameshindwa kutoa ripoti kwa kuhofia kejeli na aibu katika jamii.

Akizungumza jijini Mombasa siku ya Alhamisi, afisa huyo alikariri kuwa bila ya hamasa bora kwa jamii katika kufuata njia itakayowezesha haki kupatikana kwa waathiriwa, basi wengi wataishia kuwa na matatizo mengi ya kisaikolojia kwa kuficha matukio hayo.

“Kuna haja ya kuwapa hamasa wanaume katika jamii ili waweze kutoa ripoti kwa idara husika na mkondo wa sheria kufuatwa,” alisema Shitemi.

Vile vile, ameyataka mashirika mbali mbali ya kijamii kulipa uzito suala la dhulma za kijinsia kwa wanaume kwa kutoa mafunzo na hamasa ya mara kwa mara ili kuwawezesha kutambua vyema sheria na hatimaye kupunguza viwango vya visa hivyo visivyoripotiwa.