Muungano wa kutetea haki za kina mama na watoto katika kaunti ndogo ya Kisauni umesema utahakikisha kuwa washukiwa wa ubakaji wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Onyo hilo limetolewa na muungano huo baada ya visa vya ubakaji na unyanyasaji wa haki za watoto kuonekana kuongezeka katika eneo hilo.

Akizungumza siku ya Jumamosi katika eneo la Kisauni, Mwenyekiti wa muungano huo, Judith Uchi, alisema kuwa hatua ya kwanza ni kuhakikisha kuwa mwanamume aliyempachika mimba mwanafunzi aliyefariki akijifungua amekamatwa.

Kulingana na Uchi, wanaume wengi wamekuwa wakifichwa na familia zao wanapotekeleza kosa la ubakaji au wanapowapachika wasichana wadogo mimba.

Hata hivyo, Uchi alisema kuwa chuma chao kimotoni kwani watafuatilia visa hivyo mpaka haki ipatikane.

Mkuu wa polisi katika eneo hilo, Richard Ngatia, aliwahakikishia wanawake hao kuwa idara ya polisi inafanya kazi yake vyema huku akiwaahidi kuwa mwanamume aliyempachika mwanafunzi aliyefariki mimba atakabiliwa vikali na mkono wa sheria.