Mpangishaji mmoja eneo la Witeithie Kaunti ya Kiambu alijipata na kibarua kigumu baada ya kupigiwa simu usiku wa manane kuja kuwatawanisha wanawake wawili waliokuwa wamezua rabsha kwenye nyumba moja ya kupangisha.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wanawake hao ambao wamepangisha nyumba hapo Witeithie na ambao huishi pamoja walikuwa wametoka shughuli zao na kurejea nyumbani usiku wa manane, pale walipoanza kugombana na moshi kuzua moto walipoanza kupigana.

Inadaiwa kuwa chanzo cha vita vyao ni mwanamume aliyekuwa amewanunulia vileo kwenye baa moja na kisha kuwasindikisha hadi kwao kwa kutumia gari lake jambo ambalo liliyeyusha mioyo ya wanawake hawa na kila mmoja wao kutaka kummiliki mwanamume huyo.

Kizaazaa kilizuka pale hakuna aliyetaka kupoteza kwenye shindano hilo na kusababisha vita vikali pale mmoja wao alisikika akisema, “Niue ukitaka. Mimi tayari nina watoto wa kuniridhi, usidhani naogopa kufa!!.”

Kelele hizo ziliwaamsha wapangaji wengine na kusababisha umati wa watu kujaa pale. Mpangishaji wa nyumba hizo aliwasili na aliposhindwa kuwatawanya aliwaonya kuwa amewapa siku mbili kuhama nyumba hio ambapo aliahidi kuwarejeshea kodi yao siku iliyofuata ambapo aliwatahadharisha kuwa lazima angepiga ripoti kwenye kituo cha Polisi.

“Itabidi hawa wawili waadhibiwe ili iwe funzo kwao na kwa wapangaji wengine wenye nia ya kukosesha watu wengine amani hasa wakati wa usiku wakati kuna watoto wamelala,” alisema Mwangi Kiru mpangishaji wa nyumba hizo.

Wanawake hao walijawa na aibu pale waliingia na kujifungia pasi kutoka.