Hali ya wanawake katika kaunti ya Mombasa kushindwa kujitokeza na kupiga vita dhuluma za kingono zinazowakumba watoto katika jamii kumechangia ongezeko la visa vya ubakaji katika kaunti ya Mombasa.
Idara ya jinsia katika kaunti ya Mombasa ilisema kuwa uoga miongoni mwa wanawake wa kaunti hiyo umepelekea wanawake wengi kusalia kimya pindi wanaposhuhudia matukio ya dhuluma za kingono au dhuluma zozote zile miongoni mwa watoto katika jamii na umesababisha kukithiri kwa maswala hayo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mkurugenzi wa maswala ya kijinsia katika kaunti ya Mombasa Elvina Mzungu alisema kwamba ni lazima kwa wanawake wajitokeze ili kulipiga vita swala hilo kwa lengo la kumlinda mtoto ili asikumbane na masaibu hayo ya kudhulumiwa kingono au dhuluma za aina yoyote ile.
Elvina aliitaja mitaa ya vitongoji duni katika kaunti hiyo ya Mombasa kama inayoshuhudia visa vya watoto kudhulumiwa japo hakuna yeyote anayeripoti visa hivyo ili hatua zifaazo zichukuliwe dhidi ya wahusika.
"Tafadhalini akina mama wa Mombasa chukueni jukumu la kuwaripoti wanaowanyanyasa watoto wetu na kuwadhulumu kingono na hata kijinsia ili swala hilo kukabiliwa na wahusika wachukuliwe hatua na kusitisha visa hivyo," alisema Elvina katika mkutano wa wanawake mjini Mombasa.
Mkurugenzi huyo wa maswala ya jinsia katika kaunti ya Mombasa alisema kwamba makongamano ya kuwahusisha wanawake na jamii ya kaunti ya Mombasa kuhusu dhuluma za kijinsia miongoni mwa watoto na jinsi sheria inavyopaswa kuchukua mkondo wake utaendelea.