Hisia mbalimbali zinazidi kutolewa kutokana na hatua ya wabunge kukosa kuupitisha kuwa sheria mswadi wa usawa wa jinsia kwa mara ya pili.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Baadhi ya wanawake waliozungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Ijumaa waliwasuta wabunge wanaume kwa kile walichokitaja kama kutawaliwa na ubinafsi badala ya kuwajibika kwa mujibu wa katiba.

‘’Kama akina mama tumekasirika sana. Wanaume wamekataa kutuunga mkono ishara tosha kuwa hawako tayari kusawazisha uongozi nchini licha ya katiba kushinikiza hayo,” alisema mmoja wa wanawake hao.

Hata hivyo, wanawake hao wameapa kupambana na wanaume katika nyadhifa mbalimbali za kisiasa kwenye uchaguzi mkuu ujao, ili kuhakikisha kuwa wanaimarisha idadi yao bungeni kama njia moja ya kuwapa nguvu ya kutetea haki zoa za kikatiba.

"Njia pekee tuliyo nayo kwa sasa ni kuwania viti vya kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao ili tuongeza idadi yetu, na tuweze kukuwa na usemi unaosikika,” walisema akina mama hao.

Katika vikao vya bunge siku ya Alhamisi, wabunge 178 pekee ndio waliounga mkono mswada huo kinyume cha wabunge 233 wanaohitajika kisheria.

Hii ni licha ya Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa Cord Raila Odinga kuwarai waupitishe mswada huo.