Viongozi wanawake katika Kaunti ya Mombasa wamemshinikiza Gavana Hassan Joho kutatua mgomo wa madaktari.
Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Afiya Rama amesema mgomo huo wa madaktari umesambaratisha shughuli za kimatibabu hasa katika Hospitali kuu ya ukanda wa Pwani.
Bi Rama amesema kwamba kurudi kwa wauguzi katika hospitali na zahanati za umma kamwe hakujaleta natija yoyote kwa sekta hiyo ya afya, hasa ikizingatiwa kwamba wauguzi hao hawawezi kutoa tiba maalum wala kutekeleza majukumu ya madaktari.
Bi Rama amemsihi Gavana Joho kuingilia kati na kufanya mazungumzo na madaktari ili kuhakikisha wanarudi kazini na kuendelea kuwahudumia wagonjwa, hasusan wanawake na watoto wanaohangaika.
“Tunamuomba Gavana Joho aingilie kati swala hili la mgomo wa madaktari na kutafuta suluhu ya haraka maana wananchi wanaumia,” alisema Bi Rama.
Siku chache zilizopita, Joho alisema kwamba anapanga kukutana na madaktari na wauguzi ili kujadiliana jinsi ya kuutatatua mgogoro huo.
Wauguzi walirudi kazini siku ya Jumatano baada ya kutia saini mkataba baina yao na baraza la magavana, huku madaktari wakishikilia wataendelea na mgomo wao hadi pale watakapopata nyongeza ya mishahara na marupurupu.