Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wanawake katika Kaunti ya Mombasa wamehimzwa kukumbatia hazina za serikali zilizozinduliwa ili kuwawezesha kujihusisha na biashara ndogo ndogo ili kujikimu kimaisha.

Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Afiya Rama amesema kwamba kwa wanawake kufaulu kimaisha, lazima wajitolee kikamilifu katika makundi hayo na kufanya miradi ya kimaendeleo itakayowawezesha kuimarisha shughuli zao.

Akihutubia mkutano wa wanawake mjiji Mombasa siku ya Jumatatu, Rama alisema kwamba iwapo wanawake watachukua jukumu la kutumia hazina za serikali kuboresha biashara zao, basi watabadilisha sura ya jamii na hasa eneo nzima la pwani kwa kiwango kikubwa.

Rama alipendekeza kubuniwa kwa kitengo maalum katika serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa, cha kuwaangazia kina akina mama na miradi yao ili kuwawezesha kukuza uchumi wa taifa.

“Kuna haja ya wanawake kuzingatia biashara ndogo ndogo zitakazowawezesha kujikimu kimaisha na kutumia fursa ya hazina za serikali kubadilisha sura ya jamii na eneo zima la Pwani,” alisema Rama.

Kauli ya kiongozi huyo wa chama cha maendeleo ya wanawake Kaunti ya Mombasa imejiri huku viongozi mbalimbali wakionekana kuwashinikiza wanawake kujitokeza na kufaidika na miradi ya maendeleo kutoka kwa serikali kuu na ile ya Kaunti ya Mombasa.