Mwenyekiti wa chama cha Maendeleo ya Wanawake tawi la Nakuru amesema kuwa watafanya maandamano kupinga shinikizo la kutaka kumwondoa Waziri wa Ugatuzi Anne Waiguru mamlakani.
Akizungumza na wanahabari siku ya Jumatatu Keziah Ngina alisema kuwa kashfa ya madai ya ufisadi dhidi ya Waiguru ni propaganda ya baadhi ya watu wanaojitakia makuu.
Ngina alimtetea Waiguru kwa kusema kuwa waziri huyo sio afisaa wa ununuzi katika wizara hiyo na hivyo basi, hafai kulaumiwa kwa kupotea kwa mamilioni ya pesa katika wizara hiyo.
“Nashangaa ni vipi baadhi ya viongozi kutoka upande wa serikali na upinzani badala ya kumsaidia Waiguru kama mwanamke katika nyadhifa hiyo, wanampiga vita,” alisema Ngina.
Mwenyekiti huyo alisema kuwa Waiguru anastahili kupongezwa kwa kuwa yeye ndiye alitambua kuwa kulikuwa na pesa ambazo zilikuwa zimepotea.
“Namshauri Waziri Waiguru asidhubutu kung’atuka kutoka katika wadhifa huo,” alisema Ngina.