Share news tips with us here at Hivisasa

Muungano wa maendeleo ya wanawake nchini ukishirikiana na kamati ya kitaifa ya kukabili ufisadi umeandaa warsha ya siku tatu mjini Mombasa kuhamasisha viongozi wa makundi ya akina mama kuhusu ufisadi.

Warsha hiyo imejumuisha zaidi ya wanawake 60 kutoka kaunti zote sita za kanda ya Pwani wakiongozwa na viongozi wao.

Akiongea wakati wa uzinduzi huo, mwenyekiti wa kitaifa wa muungano huo Bi Rahab Mwikali, alisema wamechukua hatua hiyo baada ya kuona kwamba akina mama wana jukumu kubwa katika vita dhidi ya ufisadi nchini.

“Wanawake wana uwezo mkubwa kwa sababu tunaamini wakiongea kwa sauti moja, wanaweza kubadilisha taifa hili,” alisema Mwikali.

Kiongozi huyo alisema watatumia muungano huo wa wanawake kuongea na akina mama wengine kote nchini ili kufahamu jinsi ya kupambana na ufisadi.

Kwa upande wake, kaimu mkurugenzi katika kamati ya kuhamasisha wakenya kuhusu ufisadi David Gathii, alisema wamebuni kamati maalum katika kila kaunti za kukabiliana na ufisadi.

“Hizi kamati zitasaidia kutoa hamasisho karibu kabisa na wananchi katika kaunti husika na tumeamua kwamba kila mwanachama wa maendeleo ya wanawake lazima ajiunge ndani,” alisema Gathii.

Wakati huo huo, viongozi hao walichukua fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kuweka tofauti zao za kisiasa kando na kufanya kazi pamoja.