Wanawake katika eneo la Pwani wamehimizwa kujiunga na maswala ya kisiasa na kuchagia katika kuleta mageuzi hadi mashinani.
Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa Afiya Rama amesema kuwa iwapo wanawake watategemea kupewa viti maalum katika uchaguzi mkuu ujao, hakuna maguezi yoyote yatatekelezwa.
Rama alisema kuwa hatua hiyo itasaidia pakubwa katika kuwapa changamoto viongozi wa kisiasa wanaume katika maswala ya kimaendeleo.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatano, Rama alisema kwamba hali ya kutegemea uteuzi katika vyama vya kisiasa pindi uchaguzi mkuu unapowadia imewasababisha wanawake kuwa nyuma na kushindwa kuchangia miswada muhimu bungeni.
Kulingana na kiongozi huyo, iwapo wanawake watajitokeza na kugombea viti mbalimbali vya uongozi katika uchaguzi mkuu ujao, basi watakuwa na nafasi bora zaidi ya kupigania mageuzi muhimu, haswa maswala yanayomlenga mwanamke mashinani.
"Tunataka wakati huu wanawake pia wajitokeza na kujiunga na siasa ili tulete mabadiliko hadi mashinani na kuwapa viongozi wa kisiasa changamoto za uongozi,” alisema Rama.
Rama amewataka wanawake kuanza kampeni zao sasa na kuandaa kongamano za hamasa kuhusiana na maswala ya uchaguzi mashinani, ili kuhakikisha kwamba wanaingia uongozini katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao bila kupata upinzani mkali kutoka kwa wanasiasa wanaume.