Wanawake katika Ukanda wa Pwani wamehimizwa kujitokeza na kuzing’ang’ania nafasi za juu zaidi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akitoa kauli hiyo mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Afisa wa maswala ya kijinsia katika Shirika la utetezi wa haki za kibinadamu nchini la Haki Afrika, Salma Hemed amesema kwamba wanawake wamekuwa wakizipigania nafasi za chini za uongozi au kusubiri kuteuliwa na vyama ilhali wao ndio waliyo na uwezo mkubwa wa kuwapitisha viongozi.
Salma amesema kwamba ni sharti wanawake wabadili mtazamo wao wa kuwachagua viongozi na waunge mkono viongozi wanawake ili waingie uongozini kwa wingi na kuwawakilisha wanawake na jamii nzima ipasavyo.
Mwanaharakati huyo wa wanawake katika eneo la Pwani amesema kuwa wanawake ndio wanaopiga kura kwa wingi basi hawana budi ila kuwaingiza mamlakani viongozi wenzao wa kike iwapo wanahitaji mabadiliko msingi katika maswala ya maendeleo katika jamii.
"Kuna umuhimu mkubwa iwapo wanawake watajitokeza na kuwania nyadhfa za uongozi ili kuhakikisha kuwa wanabadilisho uongozi wa nchi na kuwafanyia wanawake wenzao maendeleo," alisema Salma.