Shinikizo zimezidi kutolewa kwa makundi ya akina mama kujitokeza kupiga vita ufisadi nchini ili maswala muhimu ya maendeleo kutekelezwa.
Kaimu mkurugenzi wa kamati ya kitaifa ya kuhamasisha Wakenya kuhusu ufisadi, David Gathii, amesema kuwa kamati hiyo imepanga mikakati ya kuzuru mashinani na kuwahamasisha Wakenya husasan makundi ya akina mama kufahamu mbinu za kukabiliana na ufisadi nchini.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Jumatano, Gathii alisema kuwa tayari muungano wa wanawake nchini unaendelea na kampeni hizo za hamasa, ili kupitisha ujumbe wa kusitisha ufisadi nchini na kuhakikisha kuwa mali ya umma ina lindwa na kuwasaidia Wakenya.
"Tunapanga mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa wanawake wanapata hamasa zaidi kuhusu namna ya kukabiliana na ufisadi nchini ili maswala ya maendeleo kufanikiwa,” alisema Gathii.
Mwenyekiti wa kitaifa wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake nchini Rahab Mwikali aliunga mkono kauli hiyo na kuahidi kushirikiana na wanawake nchini kupiga vita ufisadi.