Watu wenye umri wa makamu siku ya Jumatano walifikishwa mbele ya Mahakama ya Eldoret na kushtakiwa kwa kutengeneza na kuuza pombe haramu.
Kipkering Arap Samoei, Nicholus kiptoo, Rosbella Jeptanui na Pauline Cherop walishtakiwa kwa madai ya kuuza pombe haramu ialmaarufu kangara baada ya kunaswa na Polisi wa Utawala katika eneo la Turbo katika Kaunti ya Uasin Gishu.
Korti iliambiwa kwamba wanne hao walipatikana na Polisi wa Utawala wakati walipokuwa wakishika doria yao ya kawaida. Washtakiwa hao walikamatwa na lita 50 za kangara kila mmoja. Wote walikiri makosa yao mbele ya hakimu mkazi Mheshimiwa Pauline Mbulika.
Walipigwa faini ya Sh50,000 kila mmoja au kifungo cha mwaka moja gerezani. Kwa upande mwingine mwanamke mwenye umri wa kati amewekwa kizuizini kwa muda wa wiki moja baada ya kupatikana akiwa amelewa chakari.
Judith Aoko alikamatwa usiku wa tarehe 21 mwezi huu katika mji wa Eldoret na Polisi baada ya kuonekana kuwa mlevi kwa kiwango asichoweza kubeba mtoto wake wa miezi tisa.
Hakimu Mkazi Pauline Mbulika aliamuru mshukiwa Aoko kuwekwa kizuizini ili kuruhusu Maafisa wanaoshughulikia ustawi wa watoto kufanya uchunguzi na kuamua ikiwa mazingira ya nyumbani mwake kule Kamkunji ni salama kwa mtoto huyo.