Wanaume wanne wenye umri wa makamo walifikishwa mbele ya korti ya manispaa ya Eldoret na kushtakiwa kwa kuendeleza na kujenga kwa ardhi ya umma.
Ronald Shanzi, Isaiah Kunyama, David Maritim, na Thomas Onyango walishtakiwa kwa kosa la kulima na kuendeleza ardhi ya umma kinyume cha sheria katika kituo cha kibiashara cha Moiben iliyoko Kaunti ya Uasin Gishu.
Askari wa kaunti wakishirikiana na wasimamizi wa wadi katika eneo hilo waliwakamata washukiwa hao wakiendeleza ujenzi huo kwa ardhi ya umma wakati walikua wakishika doria.
Mawakili wa washukiwa hao walijaribu kuwatetea wateja wao waachiliwe huru wakidai kwamba walikuwa wameshtakiwa kwa makosa sawia na hayo katika mahakama ya Eldoret, jambo ambalo hakimu alipinga na kudai kuwa makosa hayo yalikuwa tofauti, basi kesi hiyo itaendelea mbele ya hakimu huyo.
Isaac Chemweno pia alishtakiwa pamoja na wanne hao kwa ajili ya kuwazuia askari wa kaunti kuwakamata
Wanne hao hata hivyo walikana mashtaka hayo mbele ya hakimu mkuu mkazi Nicodemus Moseti.
Shanzi, Maritim na Onyango waliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 15, huku Kunyama akiachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu 10.
Chemweno naye kwa upande mwingine aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi elfu mbili.
Kesi hiyo itasikizwa tarehe kumi na sita Julai mwaka huu.