Wanaume wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Mombasa kujibu shtaka la kumnajisi na kumuambuzika ukimwi mtoto wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 10.

Share news tips with us here at Hivisasa

Siku ya Ijumaa, afisa wa upelezi Joyce Okemo, aliambia mahakama kuwa, washukiwa hao Issack Musembi, Komu Muthini, Onesmus Mbuvi na Mutingo Kimeo wanadaiwa kutekeleza kitendo hicho kati ya Septemba mwaka jana na Aprili mwaka huu katika eneo la kitongoji duni cha Moroto.

Kulingana na afisa huyo wa upelelezi, mtoto huyo alionekana na manii (sperms) katika sketi yake ya shule jambo lililowafanya walimu wa shule hiyo kuingiwa na shaka na hatimaye kumuhoji kuhusu kisa hicho.

Walimu hao walipiga ripoti kwa maafisa wa polisi wa Kituo cha Makupa na washukiwa hao wakatiwa mbaroni mnamo Aprili 5, 2016.

Washtakiwa hao watasalia korokoroni katika Kituo cha polisi cha Makupa ili kutoa nafasi kwa uchunguzi kukamilika pamoja na kusubiri ripoti kutoka kwa daktari kuhusiana na kisa hicho.

Haya yanajiri baada ya afisa huyo wa upelelezi kuomba muda zaidi kukamilisha uchunguzi wake kabla ya kuwafungulia mashtaka ya ubakaji.