Muungano wa Jubilee tawi la Mombasa umetoa wito kwa jamii ya Mijikenda kuunga mkono chama kipya cha Jubilee Party (JP) kinachotarajiwa kuzinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta mwezi Septemba.
Mwenyekiti wa Jubilee Kaunti ya Mombasa Ali Mwatsahu amesema muungano huo unazidi kupata umaarufu Mombasa, kutokana na maendeleo yanayofanywa na serikali kuu.
“Natoa wito kwa wananchi wa Pwani haswa jamii ya Mijikenda kujitolea kuunga mkono Jubilee na kujitokeza kwa wingi kuchukua kura ili tufanye mabadiliko Mombasa,” alisema Mwatsahu.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika mahojiano na mwandishi huyu, Mwatsahu alipuuzilia mbali semi za kuwa Mombasa ni ngome ya Cord, akisema kauli hizo zimepitwa na wakati.
“Tukisema Mombasa ni ngome ya Cord, mimi hilo nalikataa,” alisema Mwatsahu.
Mwatsahu alisisitiza kuwa muungano huo ndio wenye demokrasia hivyo basi wagombea wote watakaowania nyadhfa mbali mbali watakwenda kwenye mchujo.
Kulingana na Mwatsahu, Jubilee pekee ndio itakayotoa suluhu ya matatizo yanayokumba eneo la Pwani.