Rais Uhuru Kenyatta amewapa washika dau katika sekta ya kuzuia matumizi mabaya ya dawa siku 14 kuanza kurekebisha tabia za waraibu wa dawa za kulevya.
Rais Kenyatta alisema kuwa amegadhabishwa na jinsi shughuli hiyo imecheleweshwa tangu mwezi Januari, alipoamuru kuanza kwake.
Akizungumza katika ziara yake ya huko Pwani, Rais Kenyatta alishuritisha kuanzishwa kwa makabiliano makali dhidi ya walanguzi wa mihadarati na wauzaji wa pombe haramu.
Vile vile, Kenyatta aliwashauri viongozi wa Pwani kushirikiana na wadau kukabiliana na janga hili.
Aidha, aliamrisha viongozi wa shirika la Nacada kuzuru Pwani ili kuweka mikakati ya kufanikisha shughuli hiyo.
Akizungumza siku ya Jumanne alipokagua kituo cha Miritini kilichoko katika kambi ya NYS, Mwenyekiti wa Nacada Bw John Mututho alisema kuwa atatimiza jukumu lake ili kuhakikisha janga hilo linakabiliwa vilivyo.
"Jambo hili limecheleweshwa tangu 2014 na rais hajafurahia hayo. Aliweka wazi kwamba ikiwa tutachelewa kuchukua hatua hiyo, atatuachisha kazi sote. Analitilia sana maanani swala hili na nawaambia kuwa watu watapoteza kazi wakizembea,” alisema Mututho.
Bwana Mututho alisema kuwa mahema na vyumba viwili vya kulala vitatumika kama wadi za kurekebisha tabia na waraibu wasiopungua 200 kila wiki mbili.
Alisema kuwa watatumia bidhaa na majengo yaliyoko bila kungoja vile vya kisasa ili kuwaokoa vijana wa Pwani kutoka kwa janga hilo.