Baraza la wazee wa Kaya eneo la Pwani limempa Rais Uhuru Kenyatta maasa 25 kuwaregesha walinzi wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho na mwenzake wa Kilifi Amason Kingi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wazee hao wamesema iwapo Rais Kenyatta atashindwa kurudisha walinzi hao, basi baraza hilo litawashawashi Wapwani kutompigia kura kwenye uchaguzi ujao.

Mshauri wa Kaya Rabai Shaban Ngao, amesema iwapo magavana hao hawatarudishiwa walinzi wao, basi baraza hilo halitamuunga mkono rais kwenye uchaguzi ujao.

“Kama walinzi hao hawatarudishwa ujue kwamba tutakuangusha kwenye uchaguzi ujao,” alisema Ngao.

Ngao ameshtumu vikali hatua ya magavana hao kupokonywa walinzi wao, na kuitaja kama ukiukaji wa haki zao za kikatiba.

Mbunge wa Rabai William Kamoti na Spika wa bunge la Kilifi Jimmy Kahindi pia wameripotiwa kupokonywa walinzi wao.

Haya yanajiri huku serikali kupitia idara ya polisi ikisema kuwa hatua hiyo haijachochewa kisiasa, na kwamba idara ya polisi inafanya mabadiliko ya kawaida katika ngazi za kaunti.