Waendeshaji magari pamoja na abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea Nairobi walikwama katika msongamano wa magari eneo la Gilgil kwenye barabara kuu ya Nakuru-Nairobi siku ya Jumatatu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Msongamano huo ulisababishwa na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakisafiri wakirejea mjini baada ya likizo ndefu ya Aprili pamoja na sherehe za kuadhimisha siku ya wafanyakazi.

"Niliwasili hapa saa nane alasiri na kupata msongamano. Sasa ni saa kumi na moja na sijasonga zaidi ya mita 100,” alisema Francis Sije.

"Nilitarajia haya kwa sababu ni kawaida kwa hali kama hii kushuhudiwa wakati wa likizo kama vile Pasaka na Krismasi. Nahofia kuwa msongamano huu utaathiri biashara yetu. Ningekuwa nimewasili Nairobi na kurudi Nakuru," alisema Samuel Mwaura, dereva wa matatu.

Madereva hao walisema kuwa mwingiliano kati ya watumiaji wa barabara umechagia kuwepo kwa msongamano huo.

“Hakukuwa na polisi wakuthibiti mwingiliano kati ya watumiaji wa barabara, hali iliyosababisha msongamano huo kuwa mkubwa,” alisema Mwaura.

Maafisa wa trafiki walifika kudhibiti msongamano huo wakiwa wamechelewa.