Viongozi wa walimu katika muungano wa walimu wa KNUT, tawi la Kiambu Magharibi, wameambia serikali kuwa kuacha kuorodhesha shule kulingana na matokeo ya mtihani wa kitaifa wa KCPE utaathiri vibaya masomo.
Wakizungumza katika afisi yao huko Limuru, viongozi hawa ambao pia ni walimu, walisema kuwa kuorodheshwa kwa shule hufanya walimu kutia bidii ili shule yao isiwe ya mwisho baada ya matokeo.
Akizungumza kwa niaba ya viongozi hao, Katibu Mkuu wa Knut, tawi la Kiambu Magharibi, Michael Muna alisema kuwa serikali inastahili kuketi na viongozi wa kitaifa, kabla ya kufanya mabadiliko katika sekta ya elimu, kwani mipango mingine itapelekea masomo kudorora.
“Ni muhimu serikali kupanga vikao na viongozi wa walimu ili sera zote zinazoundwa zinasaidia kuona kuwa shule, walimu na wanafunzi wanafaidika,” alisema Muna.
“Tunaona kuwa si vyema shule kuacha kuorodheshwa kwani walimu watazembea katika kazi, kwani hakutakuwa na njia ya kuonyesha bidii yao,” alisema Muna.
Zaidi ya haya, viongozi waliambia wazazi kuwa waangalifu na watoto wao msimu wa sherehe za krisimasi na mwaka mpya kwani kuna maovu mengi yanaendelea katika jamii ikiwemo utumiaji wa dawa za kulevya na ngono za kiholela.
Muungano wa walimu wa Knut, tawi la Kiambu magharibi, huwa na walimu ambao ni wanachama kutoka kaunti ndogo za Kikuyu, Kabete, Limuru na Lari ambao hutoa mafunzo kwa shule zilizo pale.